Beniel Seka
Futi ni
moja ya vipomo ambayo vimeendelea kuwepo katika mfumo wa upimaji tangu tupate
uhuru hadi sasa. Kipimo hiki kilichokuwa katika mfumo wa Kiingereza
uliojulikana kama “imperial units” bado kinatumiwa kwa kiasi kikubwa na mafundi
uashi, useremala na mafundi bomba.
Baada
ya uhuru Tanzania iliamua kutumia mfumo wa metriki ambao kigezo kikuucha urefu ni meta(m). Vigezo vingine vinavyoambatana na
meta ni milimeta (mm), sentimeta(cm) na desimeta(dm) ambavyo ni vidogo kuliko
meta. Katika mpangilio huo milimeta ndio kiwango kidogo kuliko vyote.
Vingine ni dekameta(dm), hektometa(hm)
na kilometa(km). Katika mpangilio wa ukubwa kilometa ndio kiwango kikubwa kuliko vyote.
Mfumo huu wa
metriki hutumiwa na nchi nyingi duniani. Kinachoufanya ukubalike na nchi hizo
ni urahisi ulioko katika kuhama kigezo kimoja kwenda kingine. Kutoka kigezo
kimoja kikubwa kwenda kingine cha chini kinachofuata, unazidisha kwa kumi.
Kutoka kigezo kimoja kidogo kwenda kingine cha juu kinachofuata, unagawanya kwa
kumi. Kwa mfano, kubadili kilometa kuwa hektometa, unazidisha kwa kumi, yaani kilometa moja ni
hektometa 10. Kubadili milimeta kuwa sentimeta unagawanya kwa kumi kwa kuwa milimeta 10 ni sentimeta 1.
Shule
za Tanzania hufundisha mfumo huo wa metriki. Mifumo mingine hutajwa tu kwa
ajili ya kulinganisha, lakini si kwa nia ya matumizi. Utafiti umeonesha kuwa
wanafunzi hawana tatizo na mfumo wa metriki. Walimu wengine wamekwishawapatia
hata njia za kukumbuka mpangilio ili kurahisisha kubadili kigezo kimoja hadi
kingine. Kwa mfano, sentensi: ‘Mimi sili dagaa maana daima hupata kichefuchefu
(mm,sm,dm,m,dam,hm,km)’. Pamoja na sentensi hiyo kuwa kejeli, lakini husaidia
kukumbuka uhusiano wa vigezo hivyo.
Tatizo
ni nini hasa? Tatizo lipo kwa jamii. Bado watu wengi katika jamii ya Tanzania
hawatumii mfumo huu. Kama ulivyokwishaona hapo mwanzo mwa makala hii, watu
wengi wanatambua na kutumia futi badala ya meta. Utasikia fundi seremala
akizungumzia kitanda cha futi sita kwa sita au bati la futi 10. Vigezo vingine katika
mfumo huu ni yadi, cheini, maili na inchi. Utasikia kwa mfano, fundi akisema
“nipe misumari ya inchi nne” au “bomba la nusu inchi”.
Matumizi
hayo humchanganya mwanafunzi ambaye
hakufundishwa vipimo hivyo. Mwanafunzi anaona kuwa mambo ya shuleni hayana
matumizi ndani ya jamii. Anafikiri anayojifunza shuleni ni kwa ajili ya taaluma
tu. Mazingira ya namna hiyo humfanya mwanafunzi asifurahie masomo kwa kuwa
yanaishia darasani tu.Baadhiya mafundi waliwahi kuomba mtindo wa vipimo vya
Waingereza vifundishwe sanjari na vile vya metriki.
Tatizo
jingine analokumbana nalo mwanafunzi ni kutokijua kipimo. Hajui yadi ina urefu
wa kufananishwa na kitu gani. Anajua meta inakaribia urefu toka sakafuni hadi kiunoni anapokuwa amesimama. Hajui inchi
ina urefu unaofananishwa na nini. Anajua sentimeta inalingana kwa urefu na
ukucha wa kidole gumba. Hajui futi, lakini walau hii anaiona kwenye rula
zilizotengenezwa kwa urefu huo na zinatumika darasani. Hajui maili lakini anajua
kilometa moja ni umbali kutoka wapi hadi wapi. Anajua kutoka nyumbani kwenda hadi
shuleni ni umbali wa kilometa ngapi. Yote hayo amejifunza shuleni.
Waingereza
walipotengeneza mfumo wao wa upimaji walihusisha mambo yao. Kwa mfano, wana
kizio kinachoitwa dazeni chenye dhana ya 12. Ndio sababu wakaweka kigezo cha
inchi na kusema inchi 12 ni sawa na futi moja. Neno ‘futi’ ni neno lililotoholewa
kutoka neno la kiingereza ‘foot’ ambalo lina maana ya unyayo, lakini tusiingie
huko. Ishirini ni kizio kingine walichokitumia Walikuwa na kigezo cha uzani
walichokiita ‘hundredweght(cwt)’. Tani moja ilikuwa na cwt 20.
Waliteua
yadi kuwa futi tatu. Kwa nini tatu ikatumika wanajua wao. Pengine inatokana na
misahafu. Katika mantiki hiyo ukikokotoa
unapata yadi moja ni sawa sawa na inchi 36, yaani 12 x 3. Halafu wakaja na kigezo cha cheini;
pengine kwa sababu maalum. Cheini ni yadi 22. Kisha waliteua maili kuwa na cheini
80 ambazo ni sawasawa na yadi 22 x 80 = yadi 1760. Pia kulikuwa na kigezo
kilichoitwa ‘furlong’ ambapo furlon moja ilikamilisha urefu wa futi 660 au cheini 10.
Wakati
wanatutawala walitufanya tuone kwamba vipimo vya mfumo wao vilikuwa bora zaidi.
Walitukaririsha vipimo hivyo vikaendelea kudumu ndani ya fikra za wengi
waliosoma enzi hizo. Matumizi yalifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mfumo
huo kwa sababu mfumo wa metriki haukupewa kipaumbele.
Waingereza
hao na washirika wao kama Marekani, bado wanatumia mfumo huo. Walijua fika kwamba
Watanganyika hatimaye wangekutana na huo mfumo wa metriki. Waliandaa katika
majalada ya madaftari, orodha za kubadili vipimo vyao kwenda vipimo vya
metriki. Kwa mfano:
|
Inchi
1 = sentimeta 2.54
Meta
1 = inchi 39.37
Maili
1 = kilometa 1.6
Yadi
1 = sentimeta 91.44
|
Ukokotoaji
huo kwa ajili ya kubadili ulikuwa mgumu. Hii iliwafanya baadhi ya watu
kuridhika na mfumo huo wa kiingereza na kutotilia maanani mfumo rahisi wa
metriki. Hili ndilo tatizo kubwa tulilorithi kwa hao wakoloni. Kuna wakati
baadhi ya mafundi waliomba mfumo huo urejeshwe maana wanafunzi waliomaliza
darasa la saba walikuwa wanashindwa kumudu mafunzo ya fani kadhaa za ufundi
yaliyokuwa yanatumia mfumo wa vipimo vya Waingereza. Ombi lao lilikataliwa na
sasa wanalazimisha tu. Tuendelee namna hii mpaka lini?
Kwa
wale waliozoea vipimo hivyo vya Waingereza wanaweza kuanza kulinganisha
ifuatavyo: Futi 10= meta 3; futi 8=meta 2 na nusu; futi 5= meta 1 na nusu;
inchi 4 = sm 10 na maili 5 ni sawa sawa na kilometa 8. Badala ya kutengeneza
kitanda cha futi 6 ambavyo ni karibu
meta 2, mafundi wangetengeneza vya meta 2, na kadhalika.
Viwanda
vingi hapa nchini sasa vinatengeneza bidhaa kwa vipimo vya metriki. Hata
Waingereza na washirika wao wameanza kutengeneza bidhaa zao kwa vigezo vya
metriki kuwahi soko la kimataifa. Kwa nini wewe uendelee kung’ang’nia vipimo
vyao? Nashauri uachane nao. Nenda na wakati.
END
No comments:
Post a Comment