Saturday, 27 July 2013

Mtihani wa Kuchagua Jibu sahihi ni Tatizo Kwa shule za Msingi


Beniel Seka
Mtihani wa kuchagua jibu sahihi una faida na hasara. Baadhi ya wadau, wkiwepo wanachama wa Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHIA) tayari wameshalalamika kwa viongozi wa Elimu kuhusu mtihani huo bada ya Baraza la Mitihani la Taifa kuanza kutahini Hisabati kwa kutumia mtindo huo wa kuchagua jibu sahihi. Aidha baaadhi ya waliokerwa na jambohili wameshatoa maoni yao kuhusu muundo huu wa kutahini.
 Mtihani wa aina hii una madhara mengi ukilinganisha na faida.  Baadhi ya  ya hasara ni kuwepo uwezekano wa kubuni majibu na kuruhusu mazingira ya kuibiana au kupeana majibu. Tayari  matokeo ya mtihani wa aina hii yameshasababisha kizaazaa kwa wanafunzi na walimu wa baadhi ya shule.
Hivi karibuni tumepata habari kuwa wanafunzi 41 wa Wilaya ya Newala ambao hawajui kusoma na kuandika wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari. Katika ziara yake wilayani  humo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais inayoshughulikia maadili ya viongozi, Kepteni Mstaafu, George Mkuchika, aligundua kuwa jambo hilo limefanyika katika wilaya hiyo. Alihoji inawezekanaje mwanafunzi asiyejua kusoma wala kuandika achaguliwe kuingia sekondari. “Inawezekanaje mwanafunzi akae miaka saba  bila kujua kusoma  au kuandika halafu akachaguliwa kwenda kidato cha kwanza! Kwani walimu hawatoi testi wakagundua hilo?”
Akizungumza kwa lugha kali, Waziri huyo aliwashutumu walimu kwa kuhusika na jambo hilo. Alisema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya walimu ambako wanafunzi hao  walitoka. “Inawezekana walimu wa shule hizo walihusika katika tatizo hilo. Lazima wawajibishwe.” Waziri huyo  alitoa shutuma hizo alipokuwa anahutubia wakazi wa wilaya hiyo mwishoni mwa ziara yake.
Akihojiwa na Nipashe, mmoja wa wazazi wa mwanafunzi aliyechauliwa bila kujua kusoma au kuandika alisema, “ Mimi najua kuwa mwanangu hajui kusoma wala kuandika. Kinachonisikitisha ni kwamba nimeshtakiwa kwa kutompeleka mtoto huyo sekondari baada ya kuchaguliwa. Nimeona hakuna sababu ya kumpeleka mtoto huyo sekondari kwa kuwa hatafaidi chochote. Hiyo ni kupoteza ada. Hata hivyo bado nasumbuliwa. “
Katika mazingira tofauti, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Phillip Muluge,  akiwa ziarani mkoa wa Kigoma alifahamishwa kuwepo wanafunzi waliochaguliwa kuingia sekondari wakati hawajui kusoma wala kuandika.  Naibu Waziri huyo naye aliahidi kuchukuwa hatua kali kwa wahusika. Hivi karibuni hali kama hiyo imeripotiwa katika wilaya ya Ludewa. Inawezekana kuwa wako wengi ambao bado hawajatajwa kwa wilaya nyingine na hili kizaazaa na hatari sana kwa Taifa.
Tumekuwa tunashuhudia katika televisheni zetu tangazo la shirika la Hakielimu likieleza kuwa wako wanafunzi wengi waliko shule za sekondari ambao hawajui kusoma wala kuandika. Aidha wanafunzi wengi wameonekana wana mwandikombaya usiowezaa kusomeka kirahisi. Matatizo haya yameendelea kuwepo kwa kuwa hakuna hatua za makusudi zinazoelkezwa dhidi yao. Mtihani a kuchagua jibu sahihi umeongeza ugumu wa tatizo hilo kwa kuwa matokeo yake yanaaminiwa kwa ajili ya uchaguzi kwenda sekondari bilamchakatowa ziada.
Mwanafunzi  aliyemaliza darasa la saba huchaguliwa kuingia kidato cha kwanza baada ya kufaulu Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi unaotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa. Baraza hilo lina kiwango cha ufaulu ambacho mtahiniwa akishapata alama  hiyo  (jumla ya maksi zake kwa masomo yote) au kukivuka, huhesabiwa amefaulu. Kwa mujibu wa sera ya serikali, mwanafunzi anayefaulu anastahili kwenda shule ya sekondari. Hatujasikia sera tofauti.
Mtihani huo unaofanywa mwishoni mwa darasa la saba ni wa kchagua wanafunzi kungia sekondari na si wa ufanisi. Mtihani huo hauna cheti. Cheti cha kumaliza elimu ya msingi kinatolewa kwa utaratibu mwingine. Kwa hiyo, mtihani unakuwa umemaliza kazi iliyotakiwa baada ya kutoa matkeo. Kinachobakia ni kuchagua wanafunzi kuingia shule mbalimbali zikiwepo za vipaji maalumu.
Mtihani huo wa Baraza hutumia muundo wa maswali ya kuchagua jibu sahihi. Tumekwishaona madhara ya mtihani huo hasa kwa madarasa ya chini. Mtihani wa aina hiyo unafaa zaidi kwa watu waliokomaa ili watumie muda wao kuchambua majibu. Mwanafuzi anaweza kuvuka  kiwango cha ufaulu kwa kubuni au kwa kuibia. Kama vigezo vingine havitatumika , basi mwanafunzi ana kila sababu ya kutumia mwanya huo kwenda sekondari.
 Mawaziri wetu wameahidi kuchukuwa hatua kali kwa wahusika. Hilo ni jambo zuri lakini linapaswa kufanyika kwa uangalifu. Sina uhakika kama kuna sera inayomkataza mwanafunzi kutofanya mtihani huo kama hajui kusoma wala kuandika. Kama ipo, mwalimu mkuu na wahusika wengine wana hatia. Kama haipo, inafaa kuiingiza ili tatizo hili lisitokee tena. Mwanafunzi asiyejua kusoma au kuandikwa hapaswi kufanya huo mtihani.
Katika ngazi ya sekondari, Baraza la Mitihani la Taifa hutoa mtihani wa  “maarifa” (Qualifying Test) kwa watahiniwa binafsi (wale wasiokuwa kwenye shule za sekondari zilizosajiliwa). Lengo ni kuhakikisha kwamba kabla ya kufanya mtihani wa kitaifa wa kumaliza sekondari na kutunukiwa cheti, mtahiniwa awe amefikia kiwango cha kuridhisha cha elimu hiyo. Wale wanaoshindwa kufaulu mtihani huo hawaruhusiwi kufanya mtihani huo wa cheti. Chuo Kikuu mwanafunzi haruhusiwi kufanya mtihani ikiwa itathibitishwa hajahudhuria idadi kadhaa ya mihadhara.
Kuna uwezekano pia walimu wasio na uaminifu au watoto wa sekondari, kumrubuni msimamizi kuwaandikia wanafunzi hao majibu kwa kuwa ni rahisi kuyanakili. Kama mtihani ungekuwa na maswali ya kujieleza ingewawia vigumu kufanya hivyo. Kabla ya mtihani wa Hisabati kutumia mtindo huo tulikuwa tunashuhudia wanfunzi hao wasiojua kusoma wala kuandika wakipata sifuri. Hilo limepungua sana katika mtihani wa mwaka jana (2011).
Jambo jingine la kuzingatia ni mkazo ambao mtihani huo unapewa. Bado kuna watu wengi ambao wanafanya kila wanaloweza ili watoto wao waingie sekondari. Pia viongozi wa wilaya ambazo shule zao hufanya vibaya katika mtihani huo huwajibishwa. Hofu hii huweza kuwaingiza baadhi yao kushiriki katika mbinu chafu za kupata matokeo mazuri. Vilevile shule ambazo hupeleka wanafunzi wengi sekondari huonekana bora zaidi ya zile zinazopeleka wachache.
Athari nyingine ambayo inaweza kulikumba Taifa ni walimu kupunguza ari ya kujifunza na wanafunzi pia kutomakinika katika kujifunza wakielewa kuwa mtihani ni wa kuchagua majibu. Hivi umewahi kufikiria kwamba ukimpa mwanafuzi wa darasa la nne anaweza kufanya vizuri hata kumpita wa darasa la saba, mradi tu aweke alama kwenye visanduku husika? Itakuwa balaa.
Kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala haya, mtihani wa kuchagua jibu unaweza  kusababisha kizaazaa na kufunika zile sifa za muundo huo wa mtihani. Waziri Mkuchika alipouliza kwamba wanafunzi hao walikuwa hawafanyi testi au kuandika matini (notes), alikuwa ameleta hoja nzuri. Sisi tunahoji kwamba  ni lazima mtihani huo uwepo ukizingatia gharama za kuuendesha na kuchakata matokeo? Lazima tukubali kubadilika.

End (Mwananchi)


No comments:

Post a Comment