Kipeo na Kipeuo Drs 7
HISABATI DARASA LA SABA
Ufundishaji wa Kipeo na Kipeuo
Beniel
Seka
0784498893
Kipeo na Kipeuo ni mada zinazowasumbua baadhi ya wanafunzi
na hata walimu wa shule za msingi. Wengi wenu mtakumbuka lile tangazo la
Hakielimu kuhusu yule mwalimu aliyekuwa
anababaika darasani wakati anafundisha namna ya kutafuta kipeuo cha pili
cha 144. Alitumia njia ya kutenga ambayo hakuielewa. Vilevile kuna tangazo
jingine linalohusu mwalimu mwingine akitumia njia shirikishi kuwafanya
wanafunzi waelewe njia hiyo ya kutenga
na hatimaye wakalifurahia somo.
Muhtasari wa Hisabati Shule za Msingi uliorekebishwa mwaka
2005 umepunguza upeo wa mada hiyo na kuwataka wanafunzi watumie njia ya vigawo
kutafuta vipeuo vya pili. Vilevile wanatakiwa watafute kipeuo cha pili cha
namba mraba tu. Kwa hiyo walimu wanapaswa kujua kwamba mada imeshasahilishwa
ili kuleta nafuu ya ufundishaji na ujifunzaji. Sasa wanafunzi na walimu
wanatarajiwa waanze kufurahia mada hiyo.
Baadhi ya walimu wamekuwa wakifundisha bila wanafunzi wao
kujua kama mada wanayofundishwa ina matumizi katika maisha yao . Ufundishaji unakuwa ‘mkavu’ hivyo
wanafunzi hawapati hamu ya kulifuatilia somo. Ufundishaji unaozingatia ‘mhamo
wa ruwaza’ unasisitiza kutumia uzoefu wa mwanafunzi katika kujenga mawazo
mapya. Lazima mifano ya vitu halisi vilivyopo katika uelewa au mazingira ya
mwnafunzi vitumike.
Kabla ya kujifunza vipeo, wanafunzi tayari wamejifunza eneo
la mraba. Miraba ipo sehemu nyingi kama vile vyumba, kuta za nyumba, sakafu,
bustani na mapambo. Dhana ya eneo la mraba huhitaji namba kuzidishwa kwa
yenyewe. Kujua eneo kuna manufaa kwa shughuli za kiufundi, kiuchumi na kielimu.
Kwa hiyo ni dhana yenye matumizi katika maisha.
Namba inayopatikana kwa kiuzidisha yenyewe kwa yenyewe inaitwa namba mraba. Wanafunzi wanaweza kufanya zoezi la kuandika namba
mraba zote kati ya 0 na 1000 kwa kwa kufanya: 1x1=1;2x2=4; 3x3=9; 4x4=16;
5x5=25 na kuendelea. Hivyo watambua namba mraba hizo kuwa ni: 1,4,9,16,25,36,49
na kuendelea hadi 961 ambayo ni 31x31.
Kuzidisha namba kwa yenyewe ni kuipa kipeo cha pili. Kwa
mfano, mbili kipeo cha pili ni 2x2=4. Inaandikwa 22, mbili ya kipeo ikiwekwa juu
kulia ya namba. Wanafunzi sasa wanaweza kufumbua mafumbo ya kutafuta eneo kwa
kutumia kipeo.
Kutafuta kipeuo cha
pili ni kufanya kinyume chake, yaani namba gani izidishwe kwa yenyewe izae hiyo
namba husika. Kwa mfano, 144=12x12. Namba iliyozidishwa kwa yenyewe ni 12. Kwa
hiyo kipeuo cha pili cha 144 ni 12. Kipeuo cha pili kinaandikwa kwa alama √,
kwa mfano, √144=12. Kama mwnafunzi anamudu vizuri tebo, hatapata shida
kwanammba mraba. Kwa mfano, 36=6x6; 64=8x8; 81=9x9 na kadhalika.
Vigawo vya namba vinaweza pia kutumika kwa namba mraba. Kwa
mfano, kwa kutumia vigawo 625=5x5x5x5=25x25. Kwa hiyo kipeuo cha pili cha 625
ni 25. Hali kadhalika 25 kipeo cha pili au 25x25=625.
Dhana ya kipeo inaendelezwa
kwa sehemu nadesimali. Kwa mfano, (⅓)x (⅓) ni ⅓ kipeo cha pili ambbacho
ni sawa na 1/9. Vilevile (⅜)x(⅜) ni ⅔ kipeo cha pili sawa na 9/64. Kwa namba
zilizoko katika desimali, unazidisha kama kawaida. Kwa mfano, 0.6x0.6 ni 0.6
kipeo cha pili sawa na 0.36.
Kipeo cha tatu kinaweza kufundishwa kwa kutumia dhana ya
ukubwa au ujazo. Tayari wanafunzi wanajua mchemraba na kuwa ukubwa wake
unapatikana kwa kuzidisha urefu mara upana mara kimo. Kwa kuwa urefu, upana na
kimo vimelingana unazidisha urefu mara urefu mara urefu. Namba inazidishwa kwa
yenyewe halafu kwa yenyewe tena. Namba hiyo hupewa kipeo cha tatu. Kwa mfano,
nne kipeo cha tatu ni 4x4x4=64. Inaandikwa 43=64.
Kufikia hapo wanafunzi wanaweza kupewa zoezi fupi la
kutafuta kipeo cha pili cha namba ili
iwe namba mraba na hapo hapo watafute kipeuo cha pili cha namba hiyo mraba ili
wazoee huo mchakato.
_______________________________________________________________________
Baada ya kuwapa taaluma hiyo ambayo ina matumizi katika
maisha yao tunaweza sasa kutumia hadithi kukazia maarifa na kufanya somo liwe
na mvuto ziadi. Tunaweza kuwasimulia hadithi ya Kipeo na Kipeuo Mahakamani.
Kama huna hicho kitabu, ufuatao ni ufupisho wake;
Hapo zamani za kale,
namba zilikuwa watu wa nchi iitwayo Hisabati. Kipeo ambaye alikuwa msichana na
Kipeuo ambaye ni mvulana waliishi kwenye nchi hiyo. Kazi yao ilikuwa
kubadilisha thamani za namba. Sifuri na Moja tu ndio hawakuwezekana
kubadilishwa. Namba zilichoshwa na tabia hiyo ya kubadilishwa bila ridhaa yao.
Hivyo, waliamua kwenda mahakamani kuwashtaki Kipeo na Kipeuo. Hatimaye Kipeo na
Kipeuo waliitwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao. Wote walikana mashtaka.
Hakimu aliwataka
mmojammoja kueleza alichokuwa analalamika. Kwa mfano, Mbili alisema, “Mimi ni namba tasa. Kipeo cha pili anapokaa juu kidogo mbele yangu nageuka kuwa nne.”
Upande wa washtakiwa
walimhoji, “Huoni una bahati ! Wenzako wote wanaogawanyika kwa mbili bila baki
ni shufwa. Wewe peke yako tu ndiye tasa. Si bora ujiunge na wenzako kina
Nne, Sita, Nane na Kumi. Wewe sio namba witiri bwana.” Mbili hakuwa na
maelezo ya ziada.
Mwingine aliyejieleza
ni Kumi. Yeye alilalamika kuwa kipeo cho pili anamgeuza mia. “Mimi nimeumbwa
kwa sifuri moja mbele ya moja. Nina kipindi kinachojulikana kama ‘muongo’”
Walalamikiwa walimhoji
kwa nini ajisikie vibaya. “Kwani sifuri mbili mbele yako zina ubaya gani.
Hujasikia kuwa kuna kipindi kiitwacho ‘karne’?” wakili wa Kipeo na Kipeuo
aliuliza.
“Nakataa. Siyo swali
halali” alikataa wakili wa namba.
“Endelea. Jibu swali,”
Hakimu alisema.
“Ndiyo, Mheshimiwa
Hakimu. “Sina la nyongeza.”
Kilichowashangaza
wengi waliohudhuria pale mahakamani ni jinsi Moja na Sifuri walivyosimama
kidete kuwatetea Kipeo na Kipeuo. Wao walisema vijana hao hawawabadilishi
thamani. Kipeo cha pili cha moja ni moja
na kipeuo cha pili cha moja ni moja. Hali kadhalika kwa Sifuri. Sifuri kipeo
cha pili ni sifuri na kipeuo cha pili cha sifuri ni sifuri. “Hao hawana madhara
kwetu. Tunaomba waendelee kudumu,” walisisitiza Sifuri na Moja.
Mashahidi wa
washtakiwa, kina Jometri na Aljebra
baada ya kuapa kusema ukweli na
ukweli mtupu, walieleza jinsi Kipeo na Kipeuo walivyo muhimu katika kanuni ya
Paithagorasi. Walionyesha vielelezo vyao vya pembetatu-mraba na jinsi Kipeo na
Kipeuo wanavyohusika katika kukokotoa pande zake. “Wakifungwa kanuni hiyo
itakufa,” walionya.
Baada ya kuchambua
hoja za pande zote mbili, hakimu aliwaona hawana hatia na kuwaachia huru.
Kwa hadithi hii, unahusisha Hisabati na shughuli za mahakama
ambayo pia inawafumbua macho kuhusu taratibu zake. Wanafunzi pia wanaweza
kusoma mfululizo wa vitabu hivi kwa mfano Kipeo na Kipeuo Waoana na kipeo na
Kipeuo Wapima Ukimwi kwa ajili ya burudani na kupata maarifa kutoka Nyanja
nyingine.
END
No comments:
Post a Comment