Sunday, 7 July 2013

Watoto Walilia Vitabu

Hivi karibuni mnunuzi wa vitabu alinipigia simu. Alinipigia kwa kuwa alijua nimeandika vitabu vingi vya watoto . Aliniuliza kama nimesikia kwmba kuna tamasha la vitabu mwezi Novemba, 2012. Nilimjibu kuwa sikuwa na habari. Huenda walikuweko wengine waliokuwa kama mimi. Nilifuatilia na kupata habari kuwa kulikuwa na mpango huo na tamasha hilo lilikuwa lifanyike huko Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Hatimaye tamasha lilifanyika Blue Pearl, hapo Ubungo Plaza kuanzia tarehe 25 Novemba ambapo wahudhuriaji wengi walikuwa wanafunzi.

Miaka michache iliyopita mradi wa watoto Tanzania ulifanya kozi ya waandishi wa vitabu vya aina hiyo katika Chuo cha Ualimu Marangu.Siku moja wakati mkufunzi anaendelea kutoa mada kuhusu lugha katika vitabu vya watoto, ilisikika sauti ya mlango kugongwa kwa nje. Alitazama huku na kule lakini hakuona mtu aliyegonga mlango. Alirejea kwenye ukumbi na kuendelea na mada yake.

Dakika chache baadaye mlango uligongwa tena. Mimi nikiwa msikilizaji nilikerwa na huo ukatishaji wa mada. Nilitoka ghafla kabla mtoa mada hajaamua kwenda mlangoni.Yeye aliendelea kufundisha baada ya mimi kumsaidia. Nilifungua mlango, nami vilevile sikumuona aliyegonga mlango. Nilitoka nje kabisa na kutazama pande zote. Kwa mbali niliweza kumwona mototo mmoja amejificha nikamwita, “njoo hapa mtoto.” Aliondoka na kuanza kukimbia. Kumbe kulikuwepo na wenzie wapatao kumi.

Wakiungana na wenzie kukimbia walitamka kwa nguvu, “Tunaomba vitabu. Tunaomba vitabu.” Sauti hiyo iliwafikia hata wale waliokua wanamsikiliza mtoa mada. Niliporudi kwenye ukumbi niliwaarifu kuhusu hiyo rai ambayo iliwagusa wengi.

Mratibu wa kozi alikiri kuwa jana yake,  watoto kadhaa wa Shule ya Mazoezi walitembelea eneo la ukumbi huo na kuuliza maswali kadhaa kuhusu miswada iliyokua ikijadiliwa. Mratibu aliwapa zawadi  ya vitabu baada ya kuonyesha shauku kubwa ya kusoma vitabu. Hii ikawa kichocheo kikubwa kwa watoto wengine kujitokeza kusoma vitabu.

Hapo hapo nilikumbuka Siku ya Kitabu kwa Watoto (Children’s Book Day) iliyoyosherekewa kwenye ukumbi wa Makumbusho yaTaifa (National Museum). Profesa Penina Mlama alikuwa mgeni rasmi wa heshima mwaka 1993. Profesa Mlama akishirikiana na Profesa Lihamba wa Chuo Kikuu cha Dsm, aliwafundisha watoto wimbo ufuatao:

Baba yangu naomba kitabu ; kimoja tu tafadhali
Mama yangu naomba kitabu; kimoja tu tafadhali
Kaka yangu naomba kitabu; kimoja tu tafadhali
Dada yangu naomba kitabu; kimoja tu tafadhali
Mjomba yangu naomba kitabu; kimoja tu Tafadhali
Shangazi yangu naomba kitabu; kimoja tu Tafadhali.

Waliimba wimbo kwa furaha na matumaini. Kila ninapoona kitabu kipya huwa nawakumbuka sana watoto. Wana hamu na kitabu. Je, watakiona?  Je, kuna hata mtu wa kuwaambia kipo? Hawa  wanaoshiriki ni wale wachache tu walioalikwa. Wengine, je? Tuwaambie na tuwapatie vitabu.Watoto wana hamu ya kusoma vitabu lakini hawavipati.

Kila mwaka ifikapo mwezi Septemba hufanyika tamasha la vitabu.Tamasha la mwaka huu limecheleweshwa hadi Novemba. Bila shaka kulikuwa na sababu za kufanya hivyo. Tunashukuru kwamba limekuwepo. Kama ambavyo vyombo vya habari  vilivyoripoti pamoja na uzuri wa tamasha lenyewe ni watu wachache sana waliolijua. Kwa jumla, watu wengi hawakujua kuwa kulikua na shughuli muhimu namna hiyo hapa Dar es salaam.Tamasha hilo lilifanyika mikoa mingine pia.

Kwa mara nyingine,mradi wa vitabu vya watoto (Children’s Book Project) umeandaa wiki ya usomaji ya usomaji ambayo inafikia kilele chake jumamosi tarehe 9/11/2010.Wiki hiyo imeshuhudia mashindano ya usomaji ,uchoraji,kutumia kamusi,chemsha bongo na utungaji wa hadithi kwa shule zilizopo katika programu ya usomaji zilizopo mikoa ya pwani na Dar es salaam. Aidha shule zimeshindanishwa kwenye matumizi ya uendeshaji wa maktaba na utengenezaji wa zana za kujifunzia na kufundishia.

Shughuli hizi zinafikia kilele chake katika shule ya uhuru wasichana iliyopo maeneo ya manispaa ya Ilala ambapo washindi mbalimbaliwatapewa zawadi.Kutakua na maonyesho mbalimbali  ya uhamasishaji wa usomaji. Aidha wachapishaji watakuwepo kuonyesha na kukuza vitabu kwa wale watakaohitaji huduma hiyo.Shughuli hii ni wazi kwa umma.Wazazi wa watoto walioshinda kwenye mashindano hayo wameshauriwa wawepo kwenye sherehe hiyo kuwaunga mkono watoto wao.

Mimi nimeona kwamba nizisambaze habari hizi baada ya kudokezwa.Tunalo jukumu kubwa la kukuza tabia ya usomaji. Njoo tukaone wametuandikia nini. Mimi nitakuwepo je, wewe?

Hivi karibuni gazeti la nipashe lilichapisha makala iliyohoji kuna uhaba wa vitabu.Makala hiyo ilielezea kuwa uhaba huo sasa ni wa kufikirika tu maana vitabu vimejaa kwenye ghala na maduka ya wauzaji vitabu.Tatizo ni kwamba havinunuliwi kwa sababu mbalimbali, mojawapo ya sababu ni ubinafsi uliokithiri kwa baadhi ya wale wenye dhamana ya kununua vitabu.

Vilevile umma umekua na muamko finyu wa kusoma vitabu. Ni mara chache sana utaona watu wanasoma vitabu majumbani mwao, sehemu za mapumziko na hata kwenye vyombo vya usafiri. Hii ni tofauti na wenzetu kutoka nchi za nje ambao hubeba vitabu vidogo na vikubwa kila waendapo. Kila wanapopata mwanya hutumia nafasi hiyo kujisomea. Hata usomaji wa magazeti nao unalegalega. Ukiona kikundi cha watu wanasoma,  utagundua kuwa wengi wao wansoma habari za michezo hasa mpira wa miguu na mambo ya udaku.

Mara nyingi ninapowaambia watu wanunue vitabu husema kuwa hawana watoto. Wanadhani vitabu ni vya watoto tu. Vitabu vya kujisomea ndio havinunuliwi kabisa. Utasikia mtu akisema baada ya kukitazama kitabu , “Hiki ni cha darasa la ngapi?” Wanauliza zaidi vitabu vya kiada na kama ndicho wanachotumia darasani.

Siku za karibuni TBC1 ilimhoji Mama Truphina Nsemwa wa Maktaba Kuu ya Taifa ambaye alilalamika kuhusu hali duni ya usomaji wa vitabu hapa nchini. “Ni watoto wachache tu wanafika maktaba kwa ajili ya kujisomea. Wengi wanaotumia maktaba zetu ni wale wanaojiandaa kwa mitihani tu.  Nayo BBC, London walikiri kuwa walipotembelea maktaba hiyo ya taifa walikuta watoto tu wanajisomea. Hawakuwepo watu wazima. Kwa namana hiyo tutafika tulikokusudia?


No comments:

Post a Comment