Beniel Seka
Mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi umekuwa na matatizo mengi. Hivi karibuni viongozi
kadhaa wametoa malalamiko mengi kuhusu matokeo ya mitihani hiyo inayoendeshwa
na Baraza la Mitihani la Taifa. Tatizo kubwa lililosababisha viongozi hao
kuizungumzia mitihani hiyo ni jinsi matokeo yake yanavyotumika kuwezesha
wanafunzi wasiojua kusoma au kuandikwa kujiunga na elimu ya sekondari.
Mitihani
hiyo imelalamikiwa pia na wadau mbalimbali wa elimu ambao wanaona kwamba nchi
yetu inaweza kupata wahitimu wasio na viwango vya kuridhisha ikiwa hali hii
itaendelea . Wanahoji inakuwaje mwanafunzi asome kwa miaka saba bila kujua
kuandika wala kusoma. Kinachowasikitisha zaidi ni kwamba mitihani hiyo
inawathibitisha kuwa wamefaulu na wanastahili kuendelea na masomo ya sekondari.
Tatizo hili
limejitokeza zaidi mwaka juzi (2011),
Baraza la Mitihani la Taifa lilipoanza kutahini somo la Hisabati kwa kutumia
mtindo wa maswali ya kuchagua jibu sahihi. Tayari Chama cha Hisabati Tanzania
(MAT/CHAHITA) kimeshatoa msimamo wake kupinga muundo huo wa mtihani katika somo
la Hisabati. Aidha baadhi ya walimu na wataalamu wengine wameshapendekeza kusitishwa
kwa muudo huo wa kutahini Hisabati.
“Somo la
Hisabati humhitaji mwanafunzi kuonesha njia aliyotumia kupata jibu,” alisema
mwalimu mmoja mzoefu. Kisha aliedelea kueleza, “ Kuandika jibu peke yake hakusaidii
kujua fikra alizo nazo mwanafunzi au uwezo wake wa kupangilia ufumbuzi wa
tatizo, jambo ambalo ni muhimu sana katika kuelewa somo la Hisabati.”
Ni dhahiri
kwamba mtihani huo wa kumaliza shule za msingi kwa sasa unashindwa kufanya kazi
iliyokusudiwa. Kama watahiniwa wasio na uwezo, wakiwepo wasiojua kusoma wala
kuandika, wanaweza kufaulu, basi ile nia ya kuutumia kuchagua wanafunzi bora
imefifia. Tunajiuliza: kwani lazima mtihani huo uwepo? Hakuna namna nyingine ya
kuwapata wanafunzi bora wanaostahili kuingia sekondari?
Kuna wakati
mtihani huo ulikuwa muhimu maana ulikuwa mtihani pekee hapa nchini kwa ajili ya
kuchagua wanafunzi kuingia kidato cha
kwanza katika shule za sekondari. Wakati
huo hakukuwa na shule za sekondari za
binafsi ukiacha zile za seminari ambazo zilikuwa na utaratibu wao wa kuchagua
wanafunzi wa kujiunga na shule hizo. Baadaye ziliruhusiwa shule chache za
binafsi. Hizi zilichagua wanafunzi wake baada ya zoezi la kuchagua wanafunzi wa
sekondari za serikali kumalizika.
Kuanzishwa
kwa shule nyingi za binafsi kulianza kufanya zoezi la kuchagua wanafunzi bora
liingie dosari. Shule hizo za binafsi ziliingia katika ushindani wa kuwapata
hao wanafunzi bora. Baadhi ya shule zilianza utaratibu wa kuwapa wanafunzi
waliomaliza darasa la saba mtihani kabla ya matokeo ya mtihani wa taifa
kujulikana. Kuna shule ambazo tayari zina umaarufu kiasi kwamba wanafunzi wakichaguliwa
kuingia shule hizo hukataa kuitikia ule
wa shule za serikali. Hapo shule za sekondari kwa kiasi kikubwa huwakosa wale
walioamua hivyo na husababisha uchaguzi wa pili kwa ajili ya kujaza nafasi zao.
Huenda ndio sababu baadhi ya shule binafsi hufanya vizuri zaidi ya zile za
serikali.
Hatushangai
siku hizi kusikia kwamba baadhi ya shule za binafsi zinaongoza kwa kufaulisha
wanafunzi katika mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari. Kwa hiyo hapa tunaona
kwamba wenye shule hizo wametumia mtihani mbadala kupata wanafunzi hao. Wala
hawakuhitaji kuiita mitihani yao jina la ‘kitaifa’ kupata wateja. Umaarufu wa
shule hizo ndio unafanya wanafunzi kutoka sehemu zote nchini kutafuta nafasi
katika shule hizo. Hapo ndipo wanafanya mtihani pamoja na usaili.
Kitu
kinachofanya mtihani wetu wa taifa uwe mgumu kufanikisha malengo ni gharama
kubwa za uendeshaji kuanzia kutunga, kusimamia, kusahihisha hadi kuchakata
matokeo. Baraza la Mitihani linapolalamikiwa kuhusu mtihani wa kuchagua jibu
sahihi hujitetea kuhusu gharama. Ni kweli usahihishaji unakuwa umerahisishwa
sana kutokana na kuwepo na tekinolojia inayowezesha usahihishaji kwa njia ya kompyuta.
Lakini kwani lazima kufanya mtihani wa kitaifa? Shule nyingi zinazochukuwa
wanafunzi hao ni za kata!
Kuna kanda
za kielimu. Kwani mitihani hiyo haiwezi kuendeshwa kikanda? Hili ni kwa ajili
ya kupunguza tu tatizo, lakini tukitaka kuboresha zaidi tunaweza kuiendesha kimkoa au hata ngazi ya wilaya. Hapa tuna
maana ya utunzi na hata usahihishaji. Nadhani ule mtihani wa darasa la nne
ulikuwa unatumia njia hii. Kama ulisitishwa kwa sababu za gharama za
uendeshaji, hapa nakaa kimya. Nisingependa turudie kosa.
Baada ya
matokeo ya mwaka jana (2012) kutangazwa, tumefahamishwa kuwa wale
waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza itabidi wafanye mtihani mwingine
kubaini wale wasiojua kusoma wala kuandika. Kwani hawakujulikana kabla ya
kufanya mtihani huo wa taifa? Kuna viongozi wa nchi waliwahi kuhoji
inawezekanaje mtoto amalize elimu ya msingi bila kujua kusoma na kuandika?
Tungerekebisha utaratibu huo mapema badala ya kuingia gharama za mtihani
mwingine.
Pendekezo la
mwisho ni kuachana na mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi. Tunajua kwamba
kuna mitihani ya mihula ambapo wanafunzi wanapangwa kwa nafasi zao darasani na
mzazi au mlezi kupewa matokeo kumjulisha
maendeleo ya mtoto. Najua baadhi yetu tutasema mitihani hiyo sio sanifu au haina
viwango vya kuridhisha. Kama walimu watakuwa waaminifu na kutoa haki sawa kwa
wanafunzi wote, njia hii inaweza kutoa matokeo sahihi zaidi ya yale tunayoshuhudia
wakati huu. Tunachotakiwa kufanya ni kuongeza mafunzo ya utungaji wa mitihani
kwa walimu wetu.
Labda baadhi
yenu mnajiuliza wanafunzi watakaojiunga na sekondari za vipaji watapatikanaje.
Hao watakuwa wameshaanza kujitokeza katika majaribio (testi) na mitihani ya
mihula. Katika ngazi itakayoonekana inafaa , wanafunzi hao wenye vipaji
wanaweza kupewa mtihani maalum ulio na vigezo vya kumtambua mwanafunzi kiuwezo.
Tusaidiane kuondokana na tatizo hili la mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Tunahitaji wanafunzi bora na siyo bora wanafunzi kwa mendelezo wa elimu bora
kwa ngazi zote.
END
No comments:
Post a Comment