Saturday, 27 July 2013

SOMO LA HISABATI SIYO GUMU

NA BENIEL SEKA

Somo la Hisabati limeendelea kuwa somo linalowatesa wengi. Hali ya wanafunzi kuliogopa somo hilo na kuendelea kufanya vibaya imeendelea. Tufanye nini? Hebu kwanza tuangalie simulizi hii.

Siku moja msichana aitwaye Eva na rafiki yake aitwaye Roda walikuwa wanaongea. Mwalimu mmoja aitwaye Vesika aliwakuta na kuwasalimu. Wote wawili walikuwa wanamjua Mwalimu Vesika kuwa ni mtaalamu wa Hisabati. Walionekana kumfurahia kwa namna walivyomsalimia kwa uchangamfu.

Baada ya salamu, Eva alimuuliza, “Hivi mwalimu naweza nikajua Hisabati?”
Mwalimu Vesika alimtazama kwa shauku ya kujua kulikoni. “Kwa nini usiweze? Kwani Hisabati imekufanyaje?” alimuuliza kwa huruma.

“Nimeliona kuwa ni somo gumu. Nilipokuwa shuleni sikuwahi kulipenda. Hata mwalimu nilikuwa simpendi maana alikuwa ananigombeza nilipokosea. Matokeo yake sikujiamini hata kidogo nilipokuwa nafanya mtihani.”

Roda aliyekuwa anamsikiliza mwenzake kwa makini aliongeza, “Mimi niliachana nalo nilipokuwa kidato cha pili tu. ‘Majometri’ yake na ‘makongruensi’ yake yaliniweka mahali pabaya. Nilifeli Hisabati kidato cha nne na hadi sasa sijalitafutia dawa. Kwa sasa nasikia kuna kazi ya kujiendeleza lakini inahitaji Hisabati. Sijui nitaimudu vipi.”

Mwalimu Vesika aliwatazama kwa huruma huku akikuna kichwa. “Itabidi mbadilishe msimamo wenu kuhusu Hisabati. Lazima mjenge urafiki na Hisabati. Somo la Hisabati si gumu kama baadhi ya watu wanavyodai. Kama ungekuwa umefuatilia mtaalamu mmoja wa Hisabati akielezea katika redio, televisheni na magazeti kuhusu kauli hiyo potofu, ungekuwa umeanza kuchukua hatua.”

Hapo Eva hakujizuia kutamka, “Kwa wale wanaoziweza wanasema si ngumu. Sisi ndio tunaopambana nalo, ndio tunauona ugumu wake. Naomba uniambie siri ya kufanikiwa?


“Hakuna siri. Ni suala la kulipenda, kusikiliza na kutii maelekezo na kufanya mazoezi mengi. Kwa kufanya mazoezi mengi utapenda kusoma vitabu mbalimbali ambavyo vitazidi kupanua uwezo wako wa kufikiri na kubuni njia mbadala za kufumbua matatizo. Wakati mwingine unaweza kumzidi hata mwalimu wako. Kumbuka, ulimwengu wa sasa una mitandao yenye taaluma nyingi. Unaweza  kujikuta unaenda sanjari na utandawazi. Unasemaje, Eva?”

Eva alisema, “Mwalimu hapo unatuvika vilemba vya ukoka. Mtu kama mimi niwe mtaalamu wa Hisabati. Hata intaneti inikome! Si itakuwa moja ya maajabu ya dunia, kitu ambacho hata mlima Kilimanjaro pamoja na umaarufu wake haukuweza kupewa!”

“Hapana,” Mwalimu Vesika alimkatalia, “Haitachukuwa muda mfupi, lakini inawezekana. Katika historia ya binadamu, wako watu walioanza kwa hali duni lakini kwa kujitahidi wakaweza kufanya mambo makubwa na kuishangaza dunia. Hata nyie mnaweza. Unajua mimi nilipokuwa darasa la kwanza niliwahi kurudishwa nyumbani inende na mzazikwa kuwa nilikuwa sina maendeleo mazuri katika somo la Hisabati. Mtaa mzima ulijua jambohilo. Nilifedheheka sana.”
“Ikawaje?”  Eva aliuliza kwa shauku.
“Kutofanya bidii kwangu kulitokana na mwalimu wangu kunipiga sana nilipokosea Hesabu. Hii ilinisababisha niwe mtoro. Hali ikazidikuwa mbaya.” Mwalimu Vesika alifafanua. “Ilibidi nibadilike. Nilianza kujitahidi na nilipofika darasa la nne, tayari nilikuwa nafanya vizuri kuliko baadhi ya wenzangu. Nilipofika darasa la sita nilianza kuwa tishio kwa wenzangu baada ya kuwa wa kwanza darasani kwenye mtihani wa muhula katika somo la Hesabu.”

Mara mvulana mmoja aitwaye Mika akajiunga nao. Aliwasikiliza na kusema “Mnaongelea Hisabati? Mimi kwa sasa hainipi taabu. Mwanzoni ilikuwa kasheshe. Kuna siku mwalimu alisema, “nusu mara nusu” ni “robo”. Nilishanga na kusema tangu lini ukazidisha kitu kikapungua? Ukizidisha unatakiwa kupata namba kubwa zaidi. Nusu ni kubwa kuliko robo, Hapo nilianza kufikiri hisabati inadanganya.”

Roda alidakia na kusema, “Ulibadilika lini?”

“Sikubadilika kwa muda mrefu. Nilianza utundu. Walimu walibidi wanivumilie, la sivyo ningeishia pabaya. Hatimaye waliniita Ziro, maana nilikuwa natoa majibu yasiyokubalika, yenye uchizi. Siku moja mwalimu wetu aliuliza ‘nane gawanya kwa mbili unapata nini?’ Mimi nilijibu, ‘inategemea umegawanyaje? Kwa wima au kwa ulalo?” Wanafunzi wote darasani walicheka. Wao walijua jibu ni rahisi yaani nne. Walimshngaa ‘Ziro’ alivyokuwa anamsumbua mwalimu. “Una maana gani kugawanya kwa wima?” Mwalimu alimtaka atoe maelezo.

“Nilikwenda ubaoni na kukata mstari katikati ya tarakimu hiyo 8. Kwa ulalo unapata sifuri mbili. Kwa wima unapata tatu mbili zilizogeukiana nilieleza. Tangu wakati huo walimu wakaanza kuuliza maswali kwa uangalifu. Hii ilinifanya nitumie mantiki kukabiliana na changamoto za hisabati. Nikawa nalifurahia somo.”

“ Kwa kweli kuna njia nyingi za kulipenda somo. Wengine mpaka muitwe ziro. Hii nitaisimulia popote,” alisema Eva huku akicheka.

“Njia pekee ni kuongeza kujiamini. Hisabati hufuata mantiki. Ukishaielewa dhana ni rahisi kujijengea kanuni mbalimbali zinazohusiana nazo. Vilevile unaweza kugundua njia mbadala za kufumbua matatizo. Pengine njia utakayogundua ikawa rahisi kuliko zile ulizojifunza. Utajisikia mwenye furaha sana.”

“Ni kweli kabisa, mwalimu.” Yule mvulana alikubaliana naye. “Nilipoelewa maana ya pai, kwa mfano, niliweza kuunda mwenyewe kanuni ya kukokotoa mzingo wa duara (mduara) kwa kuzidisha pai mara kipenyo. Baadaye nilikuja kuikuta kwenye kitabu. Hii iliniongezea kujiamini.”

 Kama ulivyoshuhudia mazungumzo hayo, upenzi wa somo la Hisabati ndio nguzo kuu ya kulimudu somo hilo. Ukifanya mazoezi mengi utaweza kugundua njia mbalimbai za kukabiliana na ugumu wa somo hilo na hapo hapo ukawa mgunduzi. Unangoja nini? Chukua hatua sasa.

Kisha aliendelea kusema, “Kitu cha ziada cha kufanya ni kuhudhuria kongamano, midahalo au semina mbalimbali za Hisabati. Ni muhimu kuzitafuta ili ufaidike na mawazo yatakayotolewa na wataalamu. Kwa mfano, chama cha Hisabati cha Tanzania (MAT/CHAHITA) kilifanya semina ya Hisabati huko Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Iringa kuanzia 12 Septemba hadi 17 Septemba 2011. Je, ulibahatika kuhudhuria? Mwaka jana iliafanyka tarehe 17 Septemba hadi 22Septemba katika Chuo cha Makumira, Arusha. Mwaka huu inafanyiha Mbeya mwezi huo huo wa  September.  Ni vyema basi ukafanya jitihada ya kutafuta ufadhili ili uhudhurie. Kazi kwako.


No comments:

Post a Comment