Saturday, 27 July 2013

Kwa nini sio trilioni?

Beniel Seka
Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dk William Mgimwa (Mb) katika hotuba yake ya bajeti aliyotoa bungeni tarehe 14 Juni 2012 huko Dodoma hakutaja neno trilioni hata mara moja. Pengine alikuwa na sababu maalumu za kutolitumia neno hilo. Baadhi ya waliokuwa wanamtazama kwenye televisheni na waliokuwa wanamsikiliza kwenye redio walijiuliza kwa nini amelikwepa neno hilo.
Tumemshuhudia akisema: “bilioni elfu kumi na tano” kwa maana ya 15000000000000 badala ya “ trilioni kumi na tano” au kumi na tano trilioni ili kuitofautisha na 10000000000005. Aliendelea na mtindo huo wa kutaja bilioni pale ambapo angeweza kusema trilioni. Sio kwamba alifanya makosa ila kwa nini alikuwa na msimamo huo wakati kuna neno moja  lenye maana ya bilioni elfu moja? Hata hivyo alilitumia wakati wa kuhitimisha hoja. Labda alishauriwa kufanya hivyo.
Baadhi ya watazamaji na waliokuwa wanamsikiliza walipata taabu kiasi pale ambapo elfu ilipotumika mara mbili kwa namba moja. Kwa mfano, “ bilioni elfu mbili  milioni  na tatu elfu tisini  tisini milioni(2003090000000) inasumbua kuisoma”. Hii inasomwa : “trilioni mbili bilioni tatu na milioni tisini.”  Wale waliokuwa wakiangalia matangazo hayo kupitia Star Tv na ITV waliweza kusoma maneno chini ya luninga zao yaliyokuwa yametaja namba husika kwa trilioni badala ya bilioni elfu.
Wakati wa kuwasilisha bajei ya mwaka huu wa 2013/2014, Mheshimiwa Waziri Mgimwa alilikwepa tena neno hilo hadi sehemu ya mwisho wa hotuba yake. Ilionekana wazi jinsi kuacha kulitumia kulivyomsumbua kusoma tarakimu hizo na ilimlazimu kurudia ili kueleweka. Lakini alipokuwa anafanya muhtasari alitaja neno hilo na hakusumbuka tena. Kwa mfano alisema,”Bajeti ya mwaka 2013/2014 ni zaidi ya trilioni kumi na nane”.
Wabunge waliojadili hoja ya wazirimwaka jana na waandishi wa habari walitumia neno hilo bila wasiwasi wowote. Ni neno linaloshika kasi kubwa katika bajeti yetu baada ya bajeti yetu kufikia namba ya kiwango hicho. Tulikuwa na bajeti za mamilioni, zikafuata za mabilioni na sasa tuko na bajeti za matrilioni. Sina uhakika kama Baraza la Kiswahili la Taifa  (BAKITA) limeshatoa neno mbadala kwa trilioni. Kama sio, basi litoholewe liwe rasmi.
Pengine tatizo ni namna tunavyoliandika. Linaonekana kama neno la kigeni mno. Labda lingekuwa na matamshi ya Kiswahili na kuwa tirilioni. Vilevile si vizuri kutunga neno jipya kabisa kwa sababu trilioni ina mzizi (au kiambishi awali) “tri” ambapo maana yake ni “tatu”. Ina maana tunaanza na milioni kama “moja”, inafuatiwa na bilioni (bi ikiwa na maana ya “mbili” na hatimaye trilioni. Ukiwa na milioni unazidisha kwa elfu kupata bilioni na ukiwa na bilioni unazidisha kwa elfu kupata trilioni.

Inawezekana kuwa mheshimiwa waziri alilenga watu wa kawaida na kuwaachia wasomi kutumia wenyewe neno trilioni. Ninanasema hivyo kwa kuwa kiwango cha elimu ya msingi kwa mujibu wa muhtasari wa Hisabati Darasa la Saba wa mwaka 2005 uliotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ni bilioni. Hata hivyo kiwango hicho kimewekwa kwa ajili ya ukokotoaji tu. Viwango vingine vinaweza kutumika kwa kutumia stadi hizo hizo.
Ni vyema kukumbuka namba za viwango kama ifuatavyo: Kumi ina tarakimu mbili (moja na sifuri moja). Mia moja ina tarakimu tatu (moja na sifuri mbili). Elfu  moja ina tarakimu nne (moja na sifuri tatu). Elfu kumi ina tarakimu tano (moja na sifuri nne). Laki moja ina tarakimu  sita (moja na sifuri tano). Milioni  moja ina tarakimu saba (moja na sifuri sita). Bilioni moja ina tarakimu kumi (moja na sifuri tisa). Trilioni moja ina tarakimu kumi na tatu ( moja na sifuri kumi na mbili).
Kama ulivyokwishaona, namba ya kiwango cha trilioni ni kubwa. Kuandika tarakimu kumi na tatu bila kusahau au kuchanganya tarakimu si jambo rahisi. Wengine hutenganisha namba hizo kwa alama ya mkato lakini utaratibu huo ulishapendekezwa na shirika la kimataifa la viwango (ISO) uachwe. Mapendekezo hayo yametekelezwa kwa mtaala wa Hisabati tu. Nyanja nyingine bado watumiaji hawajaanza kuutekeleza na pengine hawautaki.Mfano ni wahasibu na benki. Hawa hata usipoiweka wataiweka kulinda fani yao.
Kwa kutambua tatizo hilo, namba kubwa hufanyiwa makadirio. Kwa mfano, tunaposema  bajeti ya serikali ni shllingi za Tanzania trilioni kumi na nane hatuna maana kwamba hakuna mamilioni au mabilioni. Zinaweza kuwepo lakini kwa kuwa ziko chini ya nusu trilioni zikaachwa kutajwa kwa kukadiria trilioni ya karibu. Au pengine ilikuwa trilioni kumi na saba na bilioni mia tano au zaidi ya bilioni mia tano kwa hiyo ikakadiriwa kwa trilioni ya karibu kuwa trilioni kumi na nane.
Unaweza pia kutumia namba mchanganyiko kutaja namba kubwa kwa kukadiria. Kwa mfano, unaweza kusema shilingi trilioni kumi bilioni mia tano ni shilingi trilioni kumi na nusu. Pia namba hiyo inaweza kutajwa kwa desimali kwa kusema trilioni kumi nuka tano. Wabunge wengi waliochangia mawazo yao katika bajeti hiyo wametumia mtindo huo. Huu ni mtindo rahisi katika usomaji wa namba zenye tarakimu nyingi. Kwa mfano, namba 1367300000000 inaweza kusomwa: “trilioni moja nukta tatu sita saba tatu.”
Ningependa kutahadharisha kuhus jambo jingine linalotatanisha wakati wa kusoma namba. Kuna namba ambazo zikisomwa huweza kuandikwa tofauti na ilivyokusudiwa. Kwa mfano, “elfu kumi na moja”. Mtu anayesikiliza anaandika 10001. Kumbe aliyekuwa anasoma tarakimu ilikuwa imeandikwa 11000. Ndio sababu inashauriwa kwamba namba hiyo isomwe: “kumi na moja elfu”.Hili tumeshaliona hapo juu.
Katika muhtasari wa sekondari wanafunzi wanajifunza mada iitwayo kuandika namba kwa mtindo wa kisayansi (scientific notation or standard form). Hii huwajengea wanafunzi uwezo wa kuandika namba kubwa au ndogo sana kwa kuweka nukta baada ya tarakimu na kuandika kwa kipeo kupata kiwango cha namba. Hii hurahisisha sana kujuakiwango cha namba husika na husomwa kwa desimali. Kwa mfano, 18234000000000 huandikwa 1.8234x1013  na husomwa moja nukta nane mbili tatu nne mara kumi kipeo cha kuminna tatu. Tunajua sasa namba lkiwa  kwenye kumi kipeo cha 13 ni kiwango  cha trilioni kumi.

Mwjsho ningependa kushukuru kwa lugha yetu ya Kisahili kuwa na neno  laki maalumu kwa elfu mia. Sina uhakika kama Waingereza wanalo neno kama hilo. Tunaomba BAKITA na wataalamu wengine waendelee kutafuta istilahi kwa ajili ya kurahisisha uwasilishaji wa taarifa mbalimbali. Hili linawezekana. Tuongeze bidii.

No comments:

Post a Comment