CHAHITA ni kifupi cha Chama cha Hisabati Tanzania. Kiliundwa Januari 1966 huko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati Walimu wa Hisabati kote nchini walipokutana kujadili masuala ya Hisabati mpya. Mwaka huu chama hicho kinafanya kikao chake cha 47 huko Arusha katika Chuo Kikuu cha Makumira kuanzia tarehe 17/9/2012 hadi tarehe 22/9/2012. Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri wa Elimu TAMISEMI, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb).
Japokuwa
chama hiki kilianzishwa na wanahisabati, kwa sasa kimepanua uwigo wake na
kinamfaa mtu yeyote mwenye mapenzi na somo la Hisabati. Msukumo wa sasa ni kuendeleza juhudi za kuinua
kiwango cha uelewa na utumizi wa Hisabati katika maisha. Pia chama hicho
kimepania kuondoa fikra potofu kwamba chama hicho ni kwa walimu wa sekondari na
wahadhiri wa vyuo vikuu tu. Jitihada zinafanyika ili walimu wa shule za msingi
kushiriki maana somo hilo linaanzia shule za msingi.
MT/CHAHITA kimedumu kwa muda wote huo kutokana
na wanachama wake kuwa waadilifu na uwezo wao wa kujitolea kwa hali na
mali. Kwa mfano, viongozi wa kitaifa
wanaounda kamati kuu hukutana kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi isipokuwa mwezi
Oktoba. Hawakutani Oktoba kwa sababu
ndio tu wanakuwa wamerudi kwenye mkutano wa mwaka ambao hufanyika katikati ya
mwezi Septemba.
Kumekuwa na uelewa tofauti kuhusu chama
hiki. Wako wanaodhania kwamba chama hiki
ni kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa sekndari na vyuo tu. Ukweli ni kwamba chama hiki ni cha ngazi zote za elimu. Japokuwa wengi wanaohudhuria mkutano wa mwaka
hutoka katika shule za sekondari na hasa shule za bianfsi, mwaliko huenezwa kwa
watu wote wakiwepo walimu wa shule za msingi.
Hata hivyo juhudi za kuwahusisha walimu wa shule za msingi bado
hazijazaa matunda.
Katika Kamati ya Taifa wako wawakilishi wawili
wa shule za msingi, mmoja akitoka Dar es Salaam na mwingine mkoa wa Pwani. Viongozi wa kitaifa hawatoki nje ya Dar es
Salaam kutokana na kutokuwepo fedha za kulipia nauli ya wajumbe. Shughuli zote zinafanyika kwa njia ya
kujitolea. Mpaka sasachama hakijapata mdhamini lakini kinaendelea kutafuta.
Wako watu wanaoshangaa kwamba chama
kimekuwepo kwa miaka yote lakini hali ya somo la hisabati inaendelea kuwa
mbaya. Baadhi yao wamekilaumu chama hasa
waliposikia kwamba somo la Hisabati mwaka jana liliongoza kwa kufanya vibaya
katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambako 17% tu walifaulu somo hilo. Ukweli ni kwamba CHAHITA kimekuwa kikijaribu
kwa kila njia kupambana na tatizo hilo bila mafanikio makubwa. Kimekuwa kikiendesha semina kwa walimu,
kuendesha shindano la hisabati kwa wanafunzi na kuchapisha majarida na vitabu
kwa mada zimeonekana tata.
Kuazia mwaka2007 chama hicho
kilianza kuendesa siku ya pai iliyoanzishwa hapa Tanzania na mratibu wa
Hisabati Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka2004. Siku ya pai imekuwa mojawapoya
majukwaa ya chama hicho kuwakutanisha wadau wa Hisabati kufanya shughli
mbalmbali za kuhamasisha wanafunzi kupenda somola Hisabati.
Tatizo ni kwamba huduma hii
inawafikia watu wachache tu. Kwa mfano,
kwa ngazi ya msingi ambako ndio chimbuko la matatizo, ni wanafunzi au walimu
wachache tu wameshafikiwa. Baadhi ya
kanda za CHAHITA zimeunda kanda ndogo katika ngazi ya wilaya ili kufanikisha
azma hiyo kutokana na tatizo la umbali.
Ziko shule chache ambazo zimeunda klabu ili ziwahudumie wanafunzi vizuri
zaidi. Kwa jumla hali ni ngumu na chama
peke yake hakiwezi kufanikisha bila kupewa uwezo wa ziada pamoja na
ushirikiano.
Kutofanya vizuri katika mitihani
kunasababishwa na mambo mengi yakiwepo wanafunzi, kutolipenda somo, kutofanya
mazoezi, ukosefu wa walimu na uhaba wa vitabu. Pia baadhi ya waalimu
huwakatisha tamaa wanafunzi wenye uwezo mdogo katika somo hilo. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MEMU)
imekwishaliona tatizo hilo na inalifanyia utafiti ili hatua muafaka ziweze
kuchukuliwa kulinusuru somo na balaa iliyolikumba. Ni dhahiri kwamba juhudi hiyo itahitaji
kuungwa mkono na watu wote. Taasis ya Elimu Tanzaia (TET) imekuwa ikitoa semina
kwa baadhi ya masomo, likiwepo la
Hisabati, ambapo huwalipia wataalamu (wawezeshaji) na washiriki kujilipia nauli
na kujikimu. Hata hivyo ni walimu
wachache tu walioweza kujiunga na utaratibu huu. Wale walioweza kufanya hivyo
walionyesha kuridhika na huduma hiyo. Katika mhadhara ambao CHAHITA huuita Mhadhara wa
mwaka, Profesa Ralph Masenge wa
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Open University Of Tanzania) alishauri wadau wa
elimu kujizatiti kukabiliana na tatizo hilo sugu. Alishauri MEMU kuwamotisha
walimu ili wabakie kwenye ajira yao
badala ya kutafuta kazi nyingine zenye maslahi zaidi. Pia alishauri TET
na Baraza la Mitihani wapewe uwezo wa kutunga mitaala na mitihani
itakayoboresha somo la Hisabati ili wanafunzi wengi zaidi walipende. Walimu nao
walihimizwa kubadili aina ya ufundishaji unaomfanya mwanafunzi kukariri na
badala yake watumie njia shirikishi.
Mheshimiwa Kassim Majaliwa(wa pili toka
kushoto) akimsikiliza mwanzishi wa Siku ya Pai Tanzania akiimba wimbo wa Pai
katika uwanja wa Jangwani Shule ya Sekondari 2011.
Katika semina ya mwaka huu
washiriki waliweza kujifunza mada zinazowasumbua walimu katika kuzifundisha. Katika ngazi ya shule za
msingi walijifunza njia na mikakati mbalimbali za kufundisha na kujifunza
jometri, aljebra na maumbo ya ukumbi. Walijifunza ‘spheres’ (tufe) na
‘accounts’ (hesabu za fedha) kwa sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne. ‘Linear
Programming,Probability and Vectors’ zilifunndishwa kwa ngazi ya kidato cha
tano na sita. Pia washiriki walipata fursa ya kuona matumizi ya kompyuta katika
uwasilishaji wa mada kwa kutumia ‘power point’. Walimu kadhaa walionesha zana
za kufundishia mada tata. Profesa Ralph wa Chuo Kikuu cha Huria Tanzania
aliyetajwa hapo juu, alitoa ‘mhadhara wa mwaka’ juu ya matokeo mabaya ya Hisabati
katika mitihani ya taifa.
Mkutano huo ulipambwa kwa
nyimbo kutoka kwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Mlimani ya huko Morogoro
walioimba kusifia hisabati. Pia washiriki waliimba nyimbo za pai. Tunaamini
wale wote waliohudhuria wataeneza ujumbe kwa wale ambao hawakupata fursa ya
kuhudhuria. CHAHITA
kiko tayari kusaidiana na wote wenye nia ya kuliokoa somo hilo katika dimbwi la
matatizo. Hisabati iko katika nyanja
nyingi za maisha yako. Usisite kutoa mchango wako pale unapoweza. Inawezekana. Anza leo.
Wengine watakuunga mkono.
END
No comments:
Post a Comment