Beniel Seka
Kuna wakati
kunatokea tukio la kustaajabisha. Watu wanabakia wakiulizana kulikoni? Jambo
moja lilitokea huko Ujerumani miaka mingi iliyopita. Mtoto mmoja aitwaye Carl Friedrick
Gauss akiwa na umri wa miaka 10 alimshangaza mwalimu wake kwa uwezo wake wa
hesabu. Alionyesha kipaji chake ambacho kilishughulikiwa mapema.
Hadithi ya
mtoto huyu ilisimuliwa hivi: Siku moja mwalimu wa darasa alilokuwa anasoma huyu
mtoto, alikuwa na kazi ya kusahihisha madaftari ya wanafunzi. Aliamua kuwapa
wanafunzi kazi ya kufanya hadi amalize kusahihisha. Aliandika ubaoni hesabu
ifuatayo: 1+2+3+4+5+6+…+98+99+100=. Kwa maneno mengine, tafuta jumla ya namba
za kuhesabia hadi 100. Maana yake ni kwamba 1+2=3, na 3+3=6; 6+4=10 na
kuendelea hadi ujumlishe 100 ambayo ni namba ya mwisho katika mfululizo huo.
Mwalimu
aliwaagiza waanze na kila mmoja afanye peke yake. Sekunde chache baadaye
mwalimu aliwatazama wanafunzi. Alimuona Gauss ameketi na haandiki. Alimkaripia
na kumwambia: “Nimesema ufanye hiyo hesabu, mbona hufanyi? Umeanza utukutu wako
sio?”
“Hapana
Mwalimu. Nimekwishapata jibu,” Gauss alijibu huku anatabasamu.
“Nini? “
Mwalimu alimuuliza kwa kumkazia macho.
“Hili hapa
mwalimu,” Gauss alimuonesha. Mwalimu alishikwa na butwaa. Hakuyatarajia hayo.
“Hebu nioneshe ulivyofanya,“ Mwalimu
alimwagiza.
“Niliandika
namba zote 100 katika mstari,“ Gauss alieleza.
1+2+3+4+5…+98+99+100.
“Kisha
niliziandika tena kuanzia 100 hadi 1 kwa mstari chini ya zile za kwaza ili 100
ikae chini ya I; 99 iwe chini ya 2 na kadhalika mpaka 1 iwe chini ya 100. Ziko
namba 100.
1+ 2+ 3+…+98+99+100
100+99+98+… +
3+ 2+ 1.
Nilijumlisha
kila safu ambayo kila moja ilinipa 101,” Gauss alieleza kwa kujiamini. “Kwa
kuwa jumla ya safu ni 100, nilizidisha kwa 100 yaani 101x100 kupata 10100. Nilijua kuwa kwa
kupanga mistari miwili nimejumlisha namba zote mara mbili. Ili nipate jibu
linalotakiwa, niligawanya 10100 kwa mbili na kupata 5050.”
“Wou!”
Mwalimu alimshangaa. “Sikuwezi.”
Inaelezewa
kuwa mwalimu aliwaacha watoto wale wengine waendelee kufanya kwa njia ya
kawaida, lakini hadi kipindi kinaisha, hakuna aliyemaliza. Mwalimu aliwashauri
wazazi wake kumpeleka mtoto waokwenye shule za wenye kipaji.
Kazi ya
mtoto huyu ilizaa kanuni moja ya Hisabati itumikayo kutafuta jumla ya namba
mfululizo zenye tofauti inayofanana. Yaani, katika mfululizo huo, ukitoa ya nne
kutoka ya tano ni sawa na kutoa ya tano kutoka ya sita. Kama namba ya kwanza ni
a; tofauti sawa ni d na ikiwa namba mfululizo ziko n, kanunni hiyo inasema jumla ni nusu ya {2xa+(n-1)xd}.
Kanuni hii hufundishwa katika kidato cha tatu.
Carl
Friedrich Gauss alizaliwa mwaka1777 Brunswick huko Ujerumani. Alikuwa mtoto wa
fundi matofali. Baba yake huyo alipenda mtoto wake amrithi kwenye kazi hiyo.
Tofauti na Isaac Newton aliebobea kwenye sayansi na hisabati, Gauss alionesha
uwezo wake tangu utotoni kama ulivyoona kwenye simulizi. Vilevile inasimuliwa
kuwa akiwa na umri wa miaka minne aliweza kugundua kosa baba yake alipomlipa mfanya
kazi fedha zaidi ya alivyostahili.
Akiwa
shuleni, umahiri na ujanja wake uliwavutia wengi na hatimaye akajulikana kwa
‘Duke’ wa Brunswick ambaye alivutiwa naye. Duke huyo alimpeleka Collegium
Carolinum japo wazazi wake hawakupenda aende huko. Mwaka 1795 alienda chuoni
huko Gottingen. Akiwa chuoni hapo
hakujua asome Hisabati au Filosofia. Hatimaye Hisabati ilimkolea zaidi, hivyo
alichukuwa muda wake mwingi kukuza Hisabati na kuwa bingwa wa somo hilo.
Mwaka 1807,
Gauss aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa jumba jipya la uchunguzi (Observatory) pale
Gottingen ambako aliishi maisha rahisi yenye mazingira ya kujifunza. Alijaliwa
afya njema hadi siku chache kabla ya kifo chake.
Gauss aliandika majuzuu mengi ya ugunduzi wake. Aliandika kwa
ufupisho na kuwaacha wasomi wajazilie. Aliandika Uhakiki wa Namba Tasa (Prime
Number Theorem) ambayo ilithibitishwa miaka ya hivi karibuni. Huu uhakiki ni moja
wa sehemu ya somo la siku hizi liitwalo ‘Uchambuzi
wa Nadharia ya Namba (Analytic Theory of Numbers).
Gauss
alisababisha Hisabati kuwa na matawi zaidi
ya yale ya kawaida yaani Aljebra na Jometri. Matawi hao ni pamoja na ’Elliptic
Geometry’ na ‘Hyperbolic Geometry’. Gunduzi za Gauss zilisaidia sana
kubadili mtazamo wa Hisabati hasa kwenye kusaidia Fizikia kurahisisha dhana
zake.
Gauss
alifariki mwaka 1855 akiwa na miaka sabini na nane kama ilivyokuwa kwa Galileo
Galilei mwanasayansi mwingine mkongwe.
END.
No comments:
Post a Comment