Beniel Seka
Sayansi ya
kisasa ilianzishwa na watu waliouliza maswali a yaliyohitaji uchunguzi kuliko
ya wale waliotangulia. Kulikuwa na mapinduzi ya fikra za sayansi karne ya kumi
na sita na ile ya kumi na saba. Mwanasayansi maarufu alikuwa mmoja wa wale
walichangia sana katika mabadiliko hayo.
Galileo
Galilei alizaliwa mwaka 1564, mwaka aliofariki mtu marufu aitwaye Michelangelo. Alikufa mwaka 1642, mwaka
aliozaliwa mwanasayansi mkongwe, Isaac Newton. Baba yake alikuwa mtu maarufu wa
Florence nchini Italia. Galileo alipata elimu bora,kwanza katika uganga katika
Chuo Kikuu cha Pisa na baadaye alisoma Hisabati na Fizikia.
Ugunduzi
wake wa kwanza ni ule wa ‘pendulum’. Ukitaka kujua zaidi, funga jiwe dogo wa
kamba na unin’ginize kwenye sehemu ambapo linaweza kujongea pande zote. Sukuma
jiwe kidogo ili licheze pande zote hadi litulie kutokana na ukinzani wa hewa.
Kama kusingekuwa na hewa tukio hilo lingendelea bila kukoma.
Ugunduzi
wake wa pili uliomfanya maarufu ni uvumbuzi wa msawazo majituli (hydrostatic
balance). Pia aliunda saa ya pendulum na kipimajoto (thermometer) cha kwanza.
Alitengeneza mrija wa kioo angavu ambacho upande mmoja ulifunikwa kwa kioo cha
mviringo mithili ya balbu. Aliweka maji kama kimiminika cha kuhisi joto. Siku hizi
tunatumia zekaki. Vilevile, kwa kutumia elimu ya kupinda kwa mwanga unapopita
maada angavu tofauti, alitengeneza moja ya hadubini na darubini za kwanza. Hata
hivyo utambuzi zaidi alipewa Mdachi Jan Lippershey kwa ugunduzi wa vifaa hivi.
Huenda Galileo alichelewa kuutangaza.
Kuanzia
mwaka 1592 hadi 1610, Galileo alikuwa Mwenyekiti wa Hisabati Chuo Kikuu cha
Padua. Alikuwa mhadhiri aliyependwa sana. Ilibidi ukumbi wa kuchukua watu
takriban 2000 utengwe kwa ajili ya wahudhuriaiji wa mihadhara yake.
Kionambali
chake kilimfanya awe na wasiwasi na nadharia ya Ptolomy iliyodumu miaka mingi.
Nadharia hiyo ilisema Dunia ni kitovu ambapo sayari, nyota , jua na mwezi
huizunguka. Alianza kukubali nadharia iliyopendekezwa na Nicholas Corpenicus iliyodai
kuwa jua liko katikati na huzungukwa na dunia na sayari. Mwaka 1604 alitangaza
rasmi kukataa nadharia ya Ptolomy.
Aliikarabati
darubini yake ya mwanzo na kufanya gunduzi zilizofungua ukurasa mpya katika
historia ya astronomia. Aligundua miezi (setilaiti) 4 kati ya 11 ya sayari ya Sumbula
(Jupiter); madoa ya jua na mabadiliko ya mwonekano wa sayari ya Venus kama
yaonekanavyo yale ya mwezi wetu. Hiyo pia ilisaidia kudhihirisha wazo alivyokuwa
ametabiri Corpenicus.
Mwaka 1615
aliondolewa Padua na kurejea Florence. Kuunga mkono mawazo ya Copernicus
kulianza kumsababishia mgogoro na kanisa lake. Alipewa onyo lakini aliruhusiwa
kuandika kwa uhuru, ila alipewa masharti kuwa asihusishe masuala ya mambo
matakatifu katika maandiko hayo. Alifanya safari mbili Rome kueleza msimamo
wake kwa Papa Mtakatifu. Safari ya pili alikutana na Papa Mtakatifu Urban VIII ambaye alimkaribisha vizuri.
Alipochapisha
andiko lake liitwalo ‘Dialogue on the
Great World Systems’ (Mazungumzo ya Mifumo ya Dunia Kubwa), mwaka 1632,
aliwasha moto mkali wa kimahusiano kati yake na kanisa. Aliitwa Rome na
kushtakiwa kwa kueneza uvumi. Alilazimishwa kukiri kosa na kupewa kifungo cha
nyumbani cha maisha. Alirudi kwenye nyumba yake karibu na Florence kutumikia
adhabu yake. Aliishi pale maisha ya upweke sana. Mwaka 1637 alikuwa kipofu na
akafariki miaka mitano baadaye akiwa na miaka sabini na nane.
No comments:
Post a Comment